CHAN 2018: Rais Karia ateuliwa kuwa Kamishina mchezo wa ufunguzi

Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) limemteua Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia kuwa Kamishina wa mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Fainali ya Michuano ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN).

Mchezo wa ufunguzi utawakutanisha wenyeji timu ya Taifa ya Morocco na Mauritania mchezo ambao utafanyika Januari 13, 2018. 

Karia atasimamia mchezo huo ambao utakaofanyika Jumamosi kwenye uwanja wa nyasi asilia wa Mohamed V mjini Casablanca nchini Morocco. 

Mjumbe CHAN

Itakumbukwa kuwa hivi karibuni CAF ilimteua Karia kuwa mjumbe wa Kamati ya maandalizi ya Michuano hiyo itakayoanza kurindima Januari  13 mpaka Februari 04, 2018.

Waamuzi watakaochezesha mchezo huo ni Janny Sikazwe kutoka Zambia atakuwa muamuzi wa katikati akisaidiwa na muamuzi msaidizi namba moja kutoka Kenya Marwa Aden Range na muamuzi msaidizi namba mbili akitokea Msumbiji Arsenio Chandreque Maringula wakati muamuzi wa mezani Louis Hakizimana akitokea Rwanda.

Tayari timu zitakazoshiriki michuano hiyo zimefika Morocco kwa ajili ya mashindano hayo.